Nabii Eliya

Nabii Eliya mkaa pweke

Shirika la Wakarmeli linafahamika kwa utajiri wake na urithi wa maisha ya kiroho ambayo familia nzima ya Wakarmeli hujivunia. Watu wawili katika Biblia wamewavutia na Wakarmeli na kuwa mojawapo ya chanzo cha roho ya Wakarmeli na kuongoza historia ya maisha yao yote. Eliya, nabii wa moto wa Karmeli na  Maria, Mama wa Yesu, wamewasaidia Wakarmeli kuelewa vizuri jinsi ya kuwa watu wa tafakari na kazi; jumuiya ya sala na ya kinabii. Wakarmeli wa kwanza waliishi maisha ya kieliya kiasi kwamba walijihisi kuwa naye moja kwa moja. Hawakuwa Wakarmeli tu waliokuwa wakivutwa na nabii Eliya bali hata mahujaji wengine wengi wa kipindi kile ambao walikuwa wakiitembelea Nchi Takatifu, walikuwa wakiguswa na maisha yake. Wengi wao waliokuwa wakienda kuhiji Nchi Takatifu walikuwa wakienda kuhiji pia katika mlima Karmeli sehemu ambayo Eliya aliishi maisha ya kimonaki. Wakarmeli waliishi mlima Karmeli karibu na chemchemi ya Eliya wakitamani kuwa kama yeye. Walimchagua Eliya “mtu wa jangwa” kuwa baba yao na kiongozi wao wa kiroho.Eliya alikuwa ni mtu wa sala na aliishi katika uwepo wa Mungu akimtumikia kwa uaminifu mkubwa. Hata pale wana wa Israeli walipokengeuka, yeye alisimama imara akiitetea imani halisi ya Israeli, imani ya Mungu mmoja. Kwa maisha yake Eliya anamfundisha kila Mkarmeli jinsi ya kuishi kwa vitendo upendo na imani kwa Mungu. Alipochagua kuishi maisha ya kipweke, ni wazi alikuwa akimfundisha kila mtu njia sahihi ya kuzitawala tamaa za kimwili kwa ajili ya kuwa na moyo safi. Eliya aliishi maisha ya kifukara, maisha ya kijangwa, maisha yakipweke. Utakatifu wake wa wazi ulioonekana kwa watu wote (Soma YsB 48:1-11). Kutokana na maisha yake ya kimonaki, anaheshimiwa sana na mababa wengi wa kimonaki ambao wanamwona kuwa yeye ndiye “mwanzilishi” wa maisha hayo. Kwa upande wa Wakarmeli wanamheshimu kama baba yao wa kiroho na anatajwa katika vitabu vya liturujia vya Shirika la Wakarmeli.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.

Home

Kundi la Wakarmeli Watanzania wa kwanza lililofungua misheni 2009 Bikira Maria na Nabii Eliya katika Karmeli