Waeremiti

Waeremiti -Kundi la kwanza la wakarmeli
Muundo wa Familia ya Wakarmeli
Familia ya wakarmeli imeundwa na watu mbalimbali ambao wanavutwa na maisha ya kiroho ya wakarmeli. Kundi la kwanza ni la mafrateri (Friars). Yaani mapadre na wasio mapadre. wamonaki wa kiume, wamonaki wakaa pweke -waeremiti (hermits), Masista wa maisha ya ndani yaani wamonaki (Nuns), masista wa maisha ya kitume na walei wanaopokea Skapulari ya karmeli. Kila kundi huishi maisha ya namna yake. Lakini wote hawa wanaunganishwa na utamaduni wa maisha ya kiroho ya wakarmeli.



WAEREMITI WAKARMELI KUNDI LA KWANZA LA WAKARMELI


Waeremiti walei wa kilatini walitoka nchi za Ulaya kwenda kuishi maisha ya toba na sala Mlima Karmeli kwenye karne ya 12.

Wakarmeli wa kwanza

Maisha ya (Waeremiti) wamonaki wa kwanza katika mlima Karmeli

1. (Waeremiti) Wamonaki wa kilatini katika Mlima Karmeli

Mwaka 1192 kundi la wamonaki wa kilatini (Wakarmeli) lilionekana katika mlima Karmeli. Waeremiti hao waliojulikana kama mahujaji walitokea Ulaya, walikusanyika  pamoja karibu na "chemchem ya Elia", katika moja ya mabonde membamba ya Mlima Karmeli kwa ajili ya kufanya toba na kuishi maisha ya upweke na maombi. Walitaka kuishi ukristo wao waeremiti (hermits) wakiiga mfano wa nabii Elia mwanzilishi wa maisha ya kieremiti katika nchi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Eliya anachukuliwa kama mwanzilishi na baba wa ueremiti na umonaki. Wakarmeli walibakia wafuasi waaminifu wa Eliya ambaye ana uhusiano na Mlima Karmeli kupitia matukio ya Biblia. Katikati ya vyumba vyao  kulijengwa kanisa ambalo walijitolea kwa Bikira Maria walilijenga kwa heshima yake, Mama wa Yesu, hivyo kuendeleza hisia ya kuwa Maria ni Mama yetu kama Bibi wa mahali na kama mlezi, na wao kujulikana kwa jina lake.

Kupewa mwongozo

Kati ya mwaka 1206 na 1214 Baba Mkuu wa Yerusalemu, yaani, Patriarch wa Yerusalemu (Askofu) aliwapatia wamonaki wa kilatini (Wakarmeli) wa mlima Karmeli «Mwongozo wa Maisha». Maisha ya waeremiti katika mlima Karmeli yalikuwa ni maisha ya toba. Mlima Karmeli ulikuwa sehemu mahususi ya kutekeleza azma yao ya hija kutokana na usalama uliokuwepo mahali pale. Kiini cha safari yao katika Nchi Takatifu kilikuwa ni kufanya hija takatifu ya toba katika ardhi alipozaliwa Bwana Yesu Kristo na kumtumikia. Kwenda kuhiji kulitafsiriwa kama kitendo cha «kujiachilia» kwa ajili ya kuambatana na Bwana kama walivyofanya Mitume. Kipindi kile, mhujaji  alichukuliwa daima kama mtu mdogo kabisa katika jamii, yaani mtu asiye na usalama katika maisha yake, hivyo aliishi kwa kumtegemea Mungu zaidi. 
 2. Unyenyekevu wa kiroho
Kitendo cha kujikuta katika nchi ya kigeni kiliwafanya waishi maisha ya unyenyekevu na ya kujitoa sadaka huku wakimtegemea Mungu kwa kila jambo. Ilikuwa ni njia mojawapo ya kuachana na usalama wa kibinadamu. Imani hiyo iliwasukuma kuishi maisha ya «toba» na ya «kujitoa sadaka» muda wote wa maisha yao. Wakiwa katika mlima Karmeli wamonaki hao waliweza kuishi katika hali ya upweke, ukimya, sala huku wakilitafakari Neno la Mungu usiku na mchana. Sala walizokuwa wanamwinulia Mungu, zilikuwa ni matunda ya tafakari ya Neno la Mungu. Mzizi wa maisha yao uliwekwa katika tafakari (contemplation) na sala. Katika hali kama hiyo ni wazi walikuwa wakimwiga Yesu Kristo na Mitume ambao walikuwa ni watu wa sala na tafakari (Mdo 6:4). Kwa upande wake, Yesu alipenda kusali daima mahali palipotulia: «Lakini yeye alikuwa akijiepusha, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba» (Lk 5:16); vile vile «Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake» (Math 14:23). 
 3. Uzoefu wa waeremiti wamonaki wa kwanza
Uzoefu wa maisha ya waeremiti –wamonaki wa kwanza Wakarmeli (walei) katika mlima Karmeli ulikuwa ni wa maisha ya sala na toba vilivyofanyika katika hali ya umonaki wa kipweke. Katikati ya makazi yao walijenga kikanisa kilichowekwa wakfu kwa heshima ya Bikira Maria. Ndani ya kikanisa hicho waliweza kushiriki Ekaristi Takatifu. Walikuwa wakifanya kazi za mikono kwa ajili ya kujipatia mahitaji yao ya kila siku. Mara kwa mara walikuwa wakitoka nje ya makazi yao kwa ajili ya kwenda kuuza mazao yao. Waliishi maisha ya waeremiti kila mtu peke yake katika upweke lakini uliokuwa na viashiria vichache vya maisha ya kijumuiya. Kukutana kusali pamoja Ibada Takatifu ya Misa na kula pamoja.
 
   Mlima Karmeli

MAKUNDI YA KIEREMITI NA KIMONAKI

(Wamonaki) Waeremiti wanaoishi kijumuiya

Waeremiti wanaweza kuishi kila mtu peke yake au wanaweza kuishi kijumuiya. Kwa wale wanaoishi kijumuiya (cenobites) wanaishi katika monasteri, wanakuwa na kanuni yao na kiongozi wao.

Wanaoishi kila mtu peke yake  -waeremiti

Wapo waeremiti  wasio ishi kijumuiya (anchorites).Kila mtu huishi eneo lake na hawana uongozi wa kanuni maalum. Wanaishi maisha ya upweke tu.

Waeremiti wa kilatini (wakarmeli) walipokwenda kuishi mlima Karmeli walikuwa wanaishi eneo moja lakini kila mtu alikuwa na chumba (pango lake ) chake kwa ajili ya kuishi maisha ya upweke, ukimya, sala, toba na kujikatalia. Msingi wa wito wao ni kuishi maisha ya tafakari (Contemplative life), Kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, na ibada kwa Bikira Maria. Sifa muhimu ya wamonaki ni kuishi maisha ya upweke na ukimya. Walikuwa na viashiria vichache vya maisha ya jumuiya.

Comments

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.

Home

Kundi la Wakarmeli Watanzania wa kwanza lililofungua misheni 2009 Bikira Maria na Nabii Eliya katika Karmeli