Watakatifu

Mt. Yohana wa Msalaba (24.6.1542-14.12.1591)

YOHANE WA MSALABA  KIONGOZI WA KUMTAFUTA MUNGU


Mmistiko, Mshairi, Padre na Mwalimu wa Kanisa


 “Jioni ya maisha utahukumu juu ya upendo”(Yohana wa msalaba)

Kuzaliwa na maisha ya famila yake


Alizaliwa tarehe 24.06.1542 Fontiveros–na kupewa jina la asili la Juan de Yepes y Alvarez huko Fontiveros Avila Hispania. Baba yake aliitwa Gonzalo de Yepes na mama yake aliitwa Caterina Alvarez. Walizaliwa wakiwa watoto watatu, yeye Yohane akiwa mtoto wa tatu. Wengine ni  Luis de Yepes Álvarez, na Francisco de Yepes Álvareza. Familia yao ilikuwa maskini na  baba yake alifariki mwaka 1546 wakati Yohane akiwa bado mdogo. Hivyo mama yake alichukua jukumu la kulea familia. Waliishi kwa kuhamahama wakitafuta kazi. Toka 1548 hadi mwaka 1551 waliishi Arevalo. 

Medina del Campo
Mwaka 1551 walihamia Medina del Campo. Ni katika kipindi hicho Yohane alijifunza kujitoa sadaka. Ni katika umaskini huo na mateso hayo Yohane alijifunza kutafuta furaha si katika mambo ya dunia, bali katika Mungu. 

Shule na kazi
Kati ya mwaka 1551 na mwaka 1559 alipata elimu yake ya msingi hapo Medina del Campo.na baadae alijishughulisha na biashara mbalimbali. Alifanya kazi ya uselemala, uchoraji, ushonaji.




Akiwa na umri wa miaka 17 aliweza kutoa huduma kama nesi katika hospitali ya Bikira Maria mkingiwa wa dhambi ya asili na alifanya kazi kama akolito katika kanisa la Mt.  Magdalena.
Toka mwaka 1559 hadi mwaka 1563 alisoma masomo ya ubinadamu kwenye shule ya majesuiti pale Medina. 



Kujiunga na Karmeli


Aliingia Karmeli tarehe 24. 02. 1563 na kupata vazi la shirika na kuchagua jina la Juan de santo Matia –Yohane wa Mt. Matthias. Aliweka nadhiri za maisha ya wakfu mwaka 1564. 

Falsafa na Teolojia
Toka mwaka 1564 hadi mwaka 1568 alisoma katika Chuo kikuu cha Salamanca ambapo alisoma masomo ya sanaa, falsafa na teolojia.  



Upadrisho na kukutana na Mt. Theresa wa Avila


Alipata Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1567 pale Salamanca na kwenye Misa yake ya shukrani huko Medina akakutana na Mt. Teresa wa Avila. Mt. Theresia akamwomba wafanye juhudi za kuleta mabadiliko ndani ya shirika ili kulirudisha shirika kwenye asili yake ya sala. Baada ya kuhitimu masomo yake ya teolojia mwaka 1568 akarudi Medina del Campo.



Mabadiliko yake katika shirika
Mwaka 1568 akaikiri kanuni za zamani huko Duruelo ambako alibadilisha jina toka Yohane wa Mt. Matthias na kuwa Yohane wa msalaba.Mwaka 1571 akateuliwa kuwa mlezi wa wanovisi.


Lakini watawa wenzake waliliona wazo hilo kuwa ni hatari, wakamteka mwaka 1577 na kumfungia kwenye chumba. Alikuwa akipingwa na watawa wenzake. Katika chumba hicho upendo wake ulizidi kukua na kuwa kama moto. Hakuwa amebakiwa na kitu chochote isipokuwa Mungu peke yake. Alipata faraja kutokana na imani hiyo. Alifanikiwa kutoroka mwaka 1578. Alifanikiwa kuondoka na mashairi yake aliyoyaandika alipokuwa amefungwa. Tangu kipindi kile alianza kushirikisha upendo wake wa Mungu kwa watu wengine.



Aliwahi kuwa vika wa provinsi ya Andalusia toka mwaka 1585 hadi 1587. 



Kazi zake


Mwalimu wa sala na mwongozaji wa roho kuelekea kwenye muungano na Mungu. Aliyaelewa Maandiko Matakatifu kwa kina. Alisisitiza sana juu ya Neno wa Mungu aliyetamkwa katika ukimya.Kazi yake kubwa alifundisha jinsi ya mtu anavyoweza kuufikia ukamilifu unaoleta muungano na Mungu na hali ya maisha ya umoja na Mungu yenyewe. Muungano huu unafikiwa kwa kuweka katika vitendo fadhila za kiteolojia ambazo huitakasa nafsi.

Pando la Mlima Karmeli (Ascent of Mount Carmel)

Usiku wa giza wa nafsi (Dark night of the soul)


Wimbo wa kiroho wa nafsi (The Spiritual Canticle of the soul)

Katika usiku wa giza.


Usiku wa giza wa nafsi

Sababu za kuita giza safari ya nafsi inapoelekea kuungana na Mungu. 


Kufisha Hisia na vionjo -usiku wa kwanza

La kwanza mwanadamu inabidi afishe hisia na vionjo vya kimwili. Mtu anapofanikiwa kujinasua kutoka kwenye vionjo vya kimwili hata shetani humkimbia. Hatua hii ni sawa sawa na kupita kwenye giza. Inabidi kuachilia vitu vya muda na vya kidunia. Kuvipenda na kushikamana navyo vitu vya kidunia kunaifanya nafsi ishindwe kupokea mwanga wa kimungu. Upendo hufanya vitu vifanane, kukipenda kiumbe kuliko Mungu na kufanana na kiumbe hicho.


Kuanza kutembea kwa imani -usiku wa pili    

La pili ni kwa njia ya imani ambayo mbele ya akili ni kama giza. Baada ya kufisha vionjo na kujinasua kutoka kwenye vitu vya kidunia nafsi huingia kwenye safari ya imani. Kinachobaki ni imani. Hapa Mungu hujitokeza kwenye nafsi huanza kujionesha na kujitambulisha na kujitoa kwa nafsi. Hii kazi hufanyika kwa undani kabisa na kwa siri. Hii hupelekea usiku wa tatu.


Mungu anapoanza kujidhihirisha katika nafsi-usiku wa tatu       

La tatu ni tamati ambapo nafsi huelekea yaani Mungu mwenyewe ni kama giza. Kwa kuwa nafsi iko duniani katika mwili huu unaokufa haiweza kujua yote yanayohusiana na Mungu. Nafsi inapitia usiku huu mtatu kabla ya kuungana na Mungu. Katika hatua hii nafsi huungana na Mungu. Hapa nafsi hubadilishwa na upendo kuingia katika upendo. 



Kifo chake


Alifariki dunia tarehe 14.12.1591 huko Ubeda, Andalusia.



Kutangazwa Mtakatifu


Alitangazwa mwenye heri tarehe 25.01.1675 na Papa Klementi X na alitangazwa Mtakatifu tarehe 27.12. 1726 na Papa Benedikt XIII.

Kutangazwa Mwalimu wa Kanisa

Alitangazwa kuwa mwalimu wa Kanisa tarehe 24.8. 1926 na Papa Pius XI

Sikukuu yake

Sikukuu yake ni tarehe 14 Desemba
Aliwahi kusema kuwa mtu akiwa na kiu ya Mungu atamtafuta tu. Hii inawezekana pale mtu anapoyakataa yote yasiyohusiana na Mungu.

Wapo watu wachache sana wanaongelea upendo wa Mungu. Anasema kuwa tendo lako dogo la upendo linafaa sana kwa Kanisa. Kujivua na kujisafisha mambo ya kidunia kunapelekea mtu kuungana na Mungu yaani roho ya mwanadamu na roho ya Mungu vinakutana. Katika maisha kuna ukweli ambao ni vigumu kuuelewa. Ndipo hapo watu wengi huridhika haraka na maendeleo madogo ya kiroho, hawataki kujituma zaidi katika kujitakasa. Wengine wa woga wa kujielewa, hawajui walivyo. Wengine wana viongozi wabaya kama vipofu, hawasongi mbele. Kuna wakati wanamwekea Mungu vizingiti ili asifanye kazi yake ya kuitakasa nafsi. Tunamwokea ngumu. Kuna wengine wana uwezo mkubwa wa kusali lakini hawautumii.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.

Home

Kundi la Wakarmeli Watanzania wa kwanza lililofungua misheni 2009 Bikira Maria na Nabii Eliya katika Karmeli