Inatokana na neno la kilatini Scapulae ambalo maana yake ni mabega.
Ni vazi refu ambalo linavaliwa juu ya kanzu ya kitawa. linaangukia
mbele na nyuma. Hili ni vazi la kimonaki. Mfano Wabenedikitini,
Wadominikani wanavaa Skapulari. Inasemekana Wabenedikitini ndio
walioanza kuitumia kwenye karne ya 7 kama eproni. Matumizi yake
yalibadilika na kuwa sehemu ya vazi rasmi la Shirika mbalimbali.
Waliichukulia kama ishara ya mzigo mwepesi wa Yesu. Skapulari ni alama
ya kuwa tayari kutumikia.
2. Aina za Skapulari
Kuna aina mbalimbali za utengenezaji wa Skapulari. Kuna
Skapulari yenye vipande viwili vya kitambaa cha brown chenye picha ya
Bikira Maria wa Mlima Karmeli. Skapulari hii inapovaliwa kipande kimoja
huangukia upande wa mbele yaani kwenye kifuani na kingine kinaangukia
nyuma ya shingo yaani mgongoni. Skapulari hii inavaliwa na wale tu
wanaojiweka wakfu kwa Bikira Maria wa Mlima Karmeli katika Utawa wa Tatu.
Skapulari ndogo zenye kitambaa upande mmoja tu huvaliwa na wale wote
wenye ibada kwa Bikira Maria wa Mlima Karmeli. Skapulari hii inaweza
kuwa katika mfumo wa mwingine wa medali. Skapulari inavaliwa kwa ahadi
maalum za kiroho.
3. Maono ya Mt. Simon Stock na Skapulari ya Karmeli
Ibada kwa Skapulari –Historia, kukua na kusambaa kwa ibasa ya kiskapulari. Unapoongelea
Ibada ya Skapulari unamaanisha Skapulari ya Bikira Maria wa Mlima
Karmeli. Katika utamaduni wa maisha ya Wakarmeli, tunaelezwa kuwa Bikira
Maria alimtokea Mt. Simon Stock huko Uingereza akamwambia kuwa
wale wote wanaovaa Skapulari kwa uchaji wataokolewa moja kwa moja.
Kipindi kile Shirika lilikuwa likipita kwenye kipindi kigumu cha
mabadiliko (1247). Simon Stock –ambaye inaaminika kuwa ndiye aliyekuwa
Mkuu wa Shirika, akawa anaomba msaada wa Bikira Maria. Alitaka kuona
alama yoyote ya ulinzi wake wa karibu kwa Shirika. Mwishowe alitokewa na
Bikira Maria akiwa na Skapulari mkononi mwake na kumwambia “Yeyote anayekufa amevaa Skapulari ataokolewa katika moto wa milele”.
4. Bull “Upendeleo wa Jumamosi”
Baadaye ulisambaa waraka mmoja (wa uongo) uliodaiwa
kuandikwa na Papa Yohane XXII 03.03.1322. Katika Waraka huo
(Sacratissimo uti culmine), Papa anasema kuwa alitokewa na Bikira Maria
na kumwambia kuwa, Yeye Bikira Maria angewatoa Wakarmeli wote wanaovaa
Skapulari kutoka Purgatori siku ya Jumamosi ya kwanza toka kufariki kwao
kama watakuwa wamezingatia masharti ya: kusali Sala ya Kanisa, kuishi
maisha ya usafi wa moyo, maisha ya sala na kuvaa Skapulari kila siku,
wale wasio jua kusoma inawabidi kufunga siku zilizoamriwa na Kanisa.
5. Wakuu wa Shirika katika juhudi za kuitambua Bull
Mkutano Mkuu wa Shirika wa uliofanyika mwaka 1517
uliagiza kuwa, juhudi zifanyike ili Hati hii “ya Kipapa” itambuliwe na
Papa. Walimwomba Papa Leo X aitambue lakini alifariki kabla hajasema
chochote. Baadaye Nicholas Audet alipewa Hati na Papa Klementi VII. Hati
hiyo Ex clement ya 12.08.1530 ilihusu Bull ya Papa Yohane XXII,
ilidhibitisha maombezi ya Bikira Maria kwa Wakarmel. Baada ya kupokea
Hati hiyo Mkutano Mkuu ukatoa amri ya kuvaa Skapulari kwa ndugu wa
Skapulari kwa manufaa ya kiroho. Yohane Mbatizaji Rossi alipata Hati Ut laudes
kutoka kwa Papa Gregori XIII, 18.09.1577 iliyodhibitisha Rehema
zilizotolewa na Mapapa waliomtangulia. Ilielezea upendeleo wa Bikira
Maria kwa wale wanaovaa Skapulari. Hawa watapata ulinzi na msaada wake
wa maombezi. Katiba za Shirika zilizochapishwa mwaka 1586 chini ya
uongozi wa Yohane Mbatizaji Rossi ziliweka ibada ya kubariki Skapulari
katika pontifikare ya kuvalishwa Skapulari. Mwaka 1604 Papa Klement VIII
aliweka utaratibu wa kuwatambua ndugu wa Skapulari popote pale hata
mahali ambapo Wakarmel walikuwa hawajafika.
6. Mapapa na Skapulari
Papa Klementi VII, kwa Hati «Ex clementi Sedis Apostolicae» ya 12.08.1530 alidhibitisha Hati ya Upendeleo wa Jumamosi- Hati ya Jumamosi.
Papa Paulo III, kwa Hati «Provisionis nostrae», alidhibitisha upendeleo wa Jumamosi.
Papa Pio V, kwa Hati «Superna dispositione» alidhibitisha upendeleo wa Jumamosi, rehema na neema kwa Shirika la Wakarmel.
Papa Gregori XIII, Kwa Hati «Ut laudes»
alidhibitisha rehema za upendeleo wa Jumamosi. Aliamuru Wakarmel wavae
Skapulare muda wote usiku na mchana kwa ajili ya rehema ambazo
watazipata na kwa kuokolewa watakapo kufa.
Papa Gregori XIV, alikuwa
akivaa Skapulari kabla na baada ya kuwa Papa. Na alikuwa hali nyama
siku ya Jumatano kulingana na utaratibu wa Shirika la Karmel.
Papa Leone XI, alikuwa
akivaa Skapulari tangu mtoto. Alipochaguliwa kuwa Papa yule aliyekuwa
akimvisha mavazi ya kipapa alitaka kuiondoa Skapulari. Lakini Papa
alimkataza akisema kuwa huo uliokuwa ulinzi wa Bikira Maria. Alisema
kuacha kuivaa Skapulari ni sawa sawa kumwacha Bikira Maria. Alisema
“Niachie Maria ili Maria asiniache”.
Papa Paulo V, aliwahi kusema hivi: “Mapadri Wakarmel waruhusiwe kuhubiri kwamba, taifa la
Wakristo linaweza kwa uchaji kuamini juu ya msaada wa
Bikira Maria wa Mlima Karmel kwa roho za kaka na dada walioishi naye:
yaani, Bikira Maria atawasaidia kaka na dada wanaokufa katika upendo,
ambao maishani walikuwa wakivaa Skapulari yake…, kwa maombezi yake ya
daima, kwa sala zake za uchaji na mastahili yake, na kwa ulinzi maalum
baada ya kufa na hasa siku ya Jumamosi. Kwa hiyo picha zinazotengenezwa
au kuchorwa na wapenzi wa huyu Mama kwa njia yoyote ile hazimfanyi
Bikira Maria ashuke kwenda toharani kwa ajili ya kuzifungulie roho,
lakini roho hizi , kwa maombezi yake huchukuliwa mbinguni kutoka katika
mateso yale kwa mkono wa malaika”.
Papa Alexander VII, Mwaka 1655, siku hiyo hiyo aliyotakiwa kuingia kwenye Koklave,
Alexander VII, Msiena aliyeitwa Fabio Chigi,
alikwenda kwenye konventi ya Wakarmel wa Mt. Maria wa Transpontina, hapo
baada ya kusali, alipokea kutoka kwa Pd. Mario Venturino, Mkuu wa
Shirika (ndugu yake), Skapulari ya Maria na akaandikishwa katika kikundi
cha ndugu wa Skapulari. Akiwa na alama hii ya ulinzi wa Mama wa Mungu,
alielekea Vatikani na alichaguliwa kuwa Papa kwa msaada wa Bikira Maria
(kama inavyoweza kuaminika), siku ya Jumatano, siku iliyotengwa na
Wakarmel kwa ajili ya kumheshimu Bikira Maria Mama wa Mungu. Alikuwa na
ibada maalum kwa Bikira Maria.
7. Thamani na maana ya Skapulari
Anayepokea Skapulari huingizwa kiundani zaidi kwenye
Shirika la Karmeli. Ni alama ya upendo na ujiwekaji wakfu kwa Bikira
Maria ambaye ni Dada, Mama na mfano wa kila mfuasi wa Kristo.
Anayeipokea hufanywa kuwa mwana familia ya Wakarmeli na hivyo hutakiwa
kujibidisha kuishi maisha ya kiroho ya Wakarmeli. Kuishi katika urafiki
wa ndani na Mungu kupitia undugu na maombi. Anayeivaa hukumbushwa kuishi
maisha ya wakfu kwa Bikira Maria na hukumbushwa wajibu wa Shirika. Vile
vile hupata ulinzi kutoka kwa Bikira Maria. Hutakiwa kuishi maisha ya
sala, maombi, Alisema Papa Pio XII kuwa, Skapulari inaongea juu ya
unyenyekevu, usafi wa moyo na fadhila zote za Maria ambazo inabidi
tuzivae.
Skapulari ni ishara au alama ya:
Kutumikia -kumfuata Yesu kama Maria, mfano kamili wa wafuasi wote wa Kristo. Chimbuko la wajibu huo uko katika Ubatizo unaotufanya watoto wa Mungu. Maria anatufundisha jambo hilo.
Kuishi maisha yanayojifungua kwa Mungu na kwa kufuata mapenzi yake yanayojionesha katika maisha.
Kusikiliza Neno la Mungu katika Biblia na katika maisha, kuliamini na kuweka katika matendo matakwa yake.
Kusali daima na kutambua uwepo wa Mungu katika matukio yote.
Kuwa karibu na ndugu zetu wanaoishi katika matatizo mbalimbali.
Kutuonesha mfano wa watakatifu Wakarmeli.
Kulinda roho zetu zisichafuke
Imani ya kukutana na Mungu katika maisha ya milele kwa maombezi ya Bikira Maria.
8. Ndugu Wakarmel
Hapo zamani kulikuwepo vikundi mbalimbali vya walei
katika Shirika la Karmel. Hawa waliitwa ndugu Wakarmel. Vikundi vikubwa
vilikuwa viwili:
1. Ndugu wa joho jeupe
Kundi hili la walei waliokuwa wakivaa vazi joho jeupe
la Shirika (Mantello bianco) lilikuwepo hata kabla ya kundi la Ndugu wa
Skapulari. Walikuwa ni utawa wa tatu. Kazi yao ilikuwa ni kueneza ibada
kwa Bikira Maria kwa kuandaa maandamano wakati wa sherehe za Bikira
Maria. Walikuwa wakiungana kusali na kuimba nyimbo za Bikira Maria.
Walijishughulisha kutoa michango kwa ajili ya kutunza maeneo ya Bikira
Maria. Vaza lao lilikuwa ni joho jeupe.
2. Ndugu wa Skapulari:
Ni kundi la waamini walei wanaojibidisha kuishi
maisha ya ukamilifu wa upendo duniani katika roho ya Shirika la
Wakarmel. Kujitoa kwao kwa uhuru wanashiriki maisha ya Shirika na
kupata manufaa ya kiroho katika muungano wa ndani wa mawazo, mipango na
kazi wakiwa pamoja na Maria. Mwenye Mamlaka ya kuwaweka kisheria katika
Shirika ni Mkuu wa Shirika. Ruhusu inayotolewa na Askofu ya kuweka
nyumba ya kitawa katika jimbo lake inaendana na ruhusa ya kuweka kikundi
cha ndugu wa Skapulari. Lakini mahali pengine pasipokuwa na nyumba au
konventi, inahitajika barua ya ruhusa kutoka kwa Askofu. Wanatakiwa
kupokelewa katika Shirika na mtu mwenye mamlaka ya kufanya hivyo kwa
jina la Shirika. Kupokelewa hufanyika kwa mujibu wa taratibu za ibada
zilizowekwa na Vatikani. Lazima kujiandikisha kwenye kikundi na baadaye
hupokelewa kwa kuvalishwa Skapulari. Jina lake linaandikwa katika kitabu
cha kumbukumbu likiwa na tarehe yake ya kupokelewa. Inawabidi kuvaa
Skapulari muda wote kuonesha kushiriki katika Shirika la Wakarmel.
Lakini zaidi kushiriki sala, kushiriki Ekaristi Takatifu na kusali kila
siku Sala ya Kanisa na kusali rozari kila siku. Sikukuu yao huadhimishwa
tarehe 16 Julai.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.