Mwanzo wa matamanio ya wito wa Upadre -Pascal Mkaka Dominic
Kuzaliwa
Mimi Pascal Mkaka Dominic nilizaliwa tarehe 12/4/1993 huko Mwanza na baadae nikakulia Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara, nikiwa mtoto wa kwanza katika familia yetu. Wazazi wangu wote wapo hai na wamejitahidi kunisomesha hadi kufikia hapa nilipo.Elimu kwa ujumla
Nilianza elimu ya msingi mwaka 2001 hadi 2007 katika shule ya msingi iitwayo Miembeni A, na baada ya hapo nilichaguliwa kwenda kuendelea na masomo ya secondary, hivyo wazazi wakanipeleka Arusha na kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2008 hadi 2011 katika shule ya Star High School inayoongozwa na Mapadre wa shirika la Mitume wa Yesu.Baada ya kumaliza kidato cha nne nilichaguliwa na serikali kujiunga kidato cha tano huko Dodoma Wilayani Mpwapwa katika shule ya Mpwapwa Sekondari kwa mchepuo wa Historia, Geografia na Kiwahili (HGK). Na baada ya kuhitimu kidato cha sita kwa kufaulu vizuri nilikuja kujiunga moja kwa moja na shirika la Wakarmeli.
Mwanzo wa matamanio ya wito wa Upadre
Kiujumla huu wito wa upadre na sauti ya kumtumikia Mungu nilianza kuisikia nikiwa bado mdogo hasa darasa la pili nilipenda sana kuwa Padre, hivyo nilijiunga na chama cha watumikiaji (watumikizi) huko Bunda na badae nilikuja kuvutiwa nilipomwona Padre Dominic o. carm (enzi hizo akiwa bado ni fratel) katika mavazi yake shirika aliyokuwa ameayavaa alipokuja nyumbani katika jubilee ya wazazi wake, hapo nilipenda sana kuwa Mkarmeli ingawa alinishauli kuwa nisome na nijitahidi katika masomo yangu na tangu hapo sikuwahi kuonana nae tena hadi siku nilipofika hapa Bunju.Hivyo nilipokuwa kidato cha tano niliamua kutafuta shirika lingine, lakini nilipokuwa katika harakati hizo ndipo nilikutana na padre mkarmeli (o.c.d), hapo nikakumbuka tena shirika la Wakarmeli na nilifanyiwa taratibu zote na nikajiunga nao hivyo nikaanza safari yangu kutoka Bunda hadi Kihonda Morogoro kumbe halikuwa lile nililodhania alipokuwa padre Dominic yaani Wakarmeli (O.Carm), pia nilipokuwa huko nilikutana na mwenzangu Athanas Ngasa , lakini kutokana na hali kuwa ngumu niliamua kutafuta shirika linguine katika mtandao ndipo nilikutana na shirika la Wakarmeli (o.carm), wanaofanya kazi katika jimbo kuu la Dar es salaam nikamweleza Athanas kuwa mimi naondoka lakini naye akasema tuondoke wote, hivyo yeye akanitangulia mimi nikaja nyuma yake baadaya siku chache.
Mnamo tarehe 22/6/2014 nilifika rasmi Bunju kwa kuanza malezi nashukuru nilipokelewa vizuri na nafurahia maisha ya wito huu, zaidi namuomb Mungu azidi kunilinda na kuendeleza yale aliyoanzisha kwangu. Baada ya mwaka mmoja wa malezi nashukuru nilichaguliwa tena kuendelea na mwaka mwingine na kuanza masomo ya Tauhidi(philosofia)
Ninachokumbuka na kunisisimua
Katika maisha huwezi kusahau baadhi ya matukio yanayoleta maana mpya katika maisha. Leo hii nakumbuka kwa furaha, jinsi tulivyoanza masomo ya falsafa. Mnamo tarehe 2/11/2016 tulianza safari yetu alfajiri na mapema kutoka Bunju kuja Morogoro kwa ajili ya kuanza masomo ya Falsafa tukisindikizwa na mapadre wawili wa Shirika na sisi wanafunzi tulikuwa wanne. Mapadre waliotusindikiza ni Pd. Thomas Mtey na Pd. Victor Biramata. Mimi pamoja na mapostulanti wenzangu, Athanas Ngasa, Dickon Sambala na Deogratius Peter siku hiyo tulifurahi sana. Tulijua ndoto ya kuwa mapadre watawa Wakarmeli inapata msukumo mpya. Haikuwa ndoto bali ulikuwa ni uhalisia. Pamoja na hayo safari yetu ilikuwa na changamoto nyingi. Wakati tunaelekea Morogoro, hatukuwa na nyumba ya Shirika. Ilitubidi tufikie kwenye nyumba ya Shirika la Wamisionari wa Consolata, walitupokea vizuri na kuishi nao vyema. Mazingira mapya yalikuwa changamoto kwetu.Jioni ya siku hiyo hiyo baada ya chakula cha jioni, wanajumuiya ya Wakonsolata walitukaribisha na tukajitambulisha kisha maisha yakaendelea. Siku iliyofuata tuliendelea na usahili chuoni na hatiamaye kukamilisha taratibu zote na kuanza masomo.
Pale Consolata tulikuta mambo mengi ambayo hatukuwa tukiyafanya katika jumuiya yetu ya Wakarmeli hasa kwa namna ya pekee “social gathering” kama utamaduni wao kila baada ya mwisho wa mwezi, na pia kusherekea kumbukumbu za kila mtu katika tarehe aliyozaliwa, hayo yoteyalikuwa mageni na mapya kwetu. Lakini tunamshukuru Mungu kwani tumejuwa mengi hasa katika kuishi maisha ya jumuiya na changamoto zake. Maisha yalikuwa ya furaha na kindugu. Kusoma, kusali, michezo na kadhalika.
Masomo chuoni
Baada ya mwaka wa malezi mnamo mwezi novemba nilipewa nafasi na Shirika kuanza masomo ya falsafa (filosofia), katika chuo kikuu cha Jordan University College. Kwa mwaka wa kwanza na muhula wa kwanza hali ilikuwa ngumu kwani ndio ilikuwa mara ya kwanza kuanza kufundishwa kichuo chuo, lakini namshukuru Mungu badae nilizoea hadi sasa maendeleo yangu kitaaluma yanaendelea vizuri.Baada ya kukaa Konsolata kwa mwaka mmoja, sasa tumehamia nyumbani nyingine. Mwisho kabisa tunawashukuru Mapadre wa Consolata tulioishi nao kwa mchango wao kwetu na zaidi wale wote waliokuwa wakituhudumia na zaidi uhusiano kati ya wanafunzi wa Consolata na sisi kwani umetujengea umoja na mshikamano wa kindugu.
Mwisho kabisa namshukuru Mungu kwa afya njema anayoendelea kunijalia zaidi naomba ulinzi wake kimwili na kiroho, pia nawashukuru wazazi wangu kwa malezi yao walionipatia katika ukuaji wangu na wale wote walionisaidia hadi leo niko hapa wote Mungu awabariki katika maisha yao na awapatie heri katika yote wamuombayo.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.