Karama ya Shirika




Karama ya shirika
Karama ya shirika ni "kuishi maisha ya utii kwa Yesu Kristo". Karama hii imeundwa na mambo makuu matatu:
  • Maisha ya tafakari

  • Maisha ya kindugu na

  • Maisha ya huduma
Moyo wa karama ya Karmeli ni sala na tafakari.
Maana na matumizi ya neno «karama»
Neno «karama» ni tafsiri ya neno la kigiriki (kiyunani) - "karisma -χἀρισμα "» ambalo nalo limetokana na jina «χἀρις <; - "karis"» yaani, «neema». Ambapo karama (karisma) ina maana ya «zawadi ya kimungu» kilicho kielelezo cha neema ya Mungu anayozawadiwa mwanadamu. Daima neema ni zawadi kutoka kwa Mungu, si kipawa cha asili hata kama hakuna kipawa cha asili kisichokuwa zawadi kutoka kwa Mungu. Lakini hapa tunaongelea neema maalum. Mtume Paulo ndiye aliyelitumia mara nyingi neno karama  katika barua zake. Anatumia neno karama kama ipawa au uwezo.

Kwa mfano, anamwandikia Timotheo akimwambia hivi: "Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee" (Tim 4:14), na anaendelea kumwambia, "Kwa sababu hiyo nakukumbusha,
uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu" (2Tim 1:6).

Anachosema Mtume Paulo ni kuwa: kuishi kwa kiasi, uwezo wa kuongoza waamini na kuwafundisha maadili ya kimungu, kwa ujumla ni zawadi (karama) ya Mungu mwenyewe. Lakini karama hiyo inapatiwa nguvu ya kimamlaka kwa ajili ya kutimiza wajibu wake kwa kuwekewa mikono na wazee na Paulo.

Vile vile Mtume Paulo anawaambia Wakristo wa Rumi: «Kwa maana ninatamani sana kuwaona, nipate kuwapa karama za rohoni, ili mfanywe imara» (Rum 1:11). Ukiendelea kusoma Waraka huo huo kwa Warumi, utakuta Mtume Paulo anaeleza hivi: «Lakini karama He haikuwa kama Hie kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale
Wengi» (Rum 5:15).

Na anaitaja tena katika Rum 5:16b akisema: "bali karama ya neema ilikuja kwa ajili ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki"

Kumbe basi Karama
ni zawadi kutoka kwa Mungu kwa kanisa kwa ajili ya ulimwengu. Karama ya kila familia ya kitawa ni njia maalum ambayo wanashirika wake wanaitwa kumfuata Kristo kwa mfumo huo wa maisha.
Wakarmeli wamejaliwa zawadi -neema -karama ya kuishi maisha ya taamuli/tafakari, maisha ya undugu na maisha ya huduma.

Maisha ya tafakari -Taamuli na sala (Contemplative life)

Tafakari na sala ni moyo wa maisha katika karmeli. Familia ya wakarmeli inaamini kwamba moyo wa njia yetu ya maisha - Hii ni kwa wakarmeli wote, Mapadre, Friars, Masista wa maisha ya ndani au wa maisha ya kitume Utawa wa Tatu,  walei, au hermits - moyo wetu wa maisha ni tafakari. Mt. Yohane wa Msalaba aliwahi kueleza kwamba kutafakari ni neema ya Mungu inayotiririka katika mwanadamu. Ni kuwa na urafiki na Mungu kama alivyowahi kusema Padre Joseph Chalmers, O.Carm


Tokea siku za kwanza za uwepo wake, jumuiya ya wakarmeli ilifuata mtindo wa maisha ya taamuli. Mfumo huu umo katika muundo wake na katika thamani yake au katika tunu zake.  Jambo hili linaonekana wazi katika Kanuni yake ambayo inaeleza kuwa jumuiya ya wakarmeli kama jumuiya ambayo imejielekeza moja kwa moja katika sala na kuwa makini kwa Neno, ikimwadhimisha na kumsifu Bwana kwa juhudi zote .

Neno tafakari au taamuli linaweza kuelezeka kwa ufasaha kuwa ni kutazama na kuona kwa macho ya kiroho uhalisia wa kimungu, kama asemavyo mzaburi: «Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, niamkapo nishibishwe kwa sura yako» (Zab 17:15). Ni ile hali ya kutambua uwepo wa Mungu katika maisha.



Hivyo kuishi maisha ya tafakari ni kuishi katika uwepo wa Mungu na kuwa naye ana kwa ana. Msingi wa tafakari ni Neno la Mungu ambalo humtakasa anayelisoma na kuliishi kwa kuwa ndilo Kweli: «Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli» (Yoh 17:17).



Lakini Neno hasa ni Kristo mwenyewe kama tunavyosoma kuwa:«Hapo mwanzo kulikuwako Neno naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu» (Yoh 1:1), «Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana wa pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli» (Yoh 1:14). Kumtafakari Neno Aliye Hai ni kuutafakari utukufu wa Yesu Kristo ambaye hututakasa ili maisha yetu yaweze kufanana na ya kwake.



Hivyo maisha ya tafakari katika Karmeli ni kile kipawa anachojaliwa mtu na Roho Mtakatifu cha kutafuta kuishi maisha ya muungano na Mungu[1]. Japokuwa karama zote tatu haziwezi kutenganishwa, bado kwa namna fulani msisitizo unawekwa kwenye karama ya maisha ya tafakari kwani ndicho kiini hasa cha karama nyingine mbili.



Tangu mwanzoni kabisa mwa ukarmeli, wazee wetu waliishi hii karama pale mlima Karmeli kwa kuyaelekeza maisha yao yote katika kulisoma na kulitafakari Neno la Mungu na kuliishi.



Uzoefu wa namna hiyo unaoneshwa na Samweli. Mwandishi wa kitabu cha kwanza cha Samweli anasema kuwa, tangu Samweli alipolifahamu Neno la Bwana alilifanya kuwa sehemu muhimu sana katika maisha yake: “Samweli akakua, naye Bwana alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lolote lianguke chini” (1Sam 3:19). Ndiyo maana hata Mzaburi anasema: “Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu” (Zab 119:105).



Kwa kuwa karama hii inahitaji ukimya wa ndani, na ukimya wa ndani mara nyingi husaidiwa na utulivu wa nje,  basi jumuiya  za kikarmeli hutakiwa kuishi katika mazingira tulivu na ya kisala zaidi.  Neno la Mungu linapogeuka sala basi ndipo hapo jumuiya nzima husali masifu ya Bwana kwa sauti moja ya kumsifu na kumtukuza.

Mtu hawezi kumsifu na kumtukuza Mungu kama bado hajaguswa na nguvu za Neno lake. Ndipo hapo utagundua kuwa karama ya tafakari humwongoza mtu kuingia katika fumbo la uwepo wa Mungu na hivyo kuutambua ukuu wake na maajabu anayoyafanya katika maisha ya watu. Neno la Mungu limewabadilisha watu wengi.



Utakuta basi kuwa jumuiya za kikarmeli huundwa na watu ambao wanataka kujiachilia ili waweze kuwa makao ya Roho Mtakatifu ambaye huwabadilisha kwa vipaji vyake ambavyo ni; usafi wa moyo, mawazo matakatifu, haki, upendo, imani, na tumaini imara katika wokovu.



Maisha ya tafakari yanamwezesha Mkarmeli kufanya kazi zake katika hali ya amani na  utulivu wa ndani kama Mtume Paulo anavyosema: «Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe» (2The 3:12).



Tafakari huanza pale tunapojiaminisha kwa Mungu ambaye hutujia kwa njia yoyote ile anayoichagua yeye mwenyewe. Kwa namna hiyo, maisha ya tafakari ni mwelekeo wa ndani au tabia ya kuufungua moyo wote kwa Mungu. Lakini ni Neno la Mungu ambalo humpatia mwanadamu mwanga ambao huufungua moyo wake: «Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili; tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo» (Ebr 4:12).   



Jambo hilo hutufanya tutambue uwepo wake mahali popote katika maisha yetu. Hivyo basi karama ya maisha ya tafakari ni safari ya kiroho na ya ndani kabisa ya nafsi ya kila mkarmeli anayeungana na Mungu kiroho.



Mungu ndiye anayemgusa kila Mkarmeli na kumbadilisha kuelekea maisha ya umoja wa kimapendo pamoja naye. Anamuinua kila aliyetayari kujiachilia ili aweze kuonja bure furaha kamili ya kupendwa na Mungu  na kuishi katika uwepo wake wa kimapendo.



Kwa jinsi hiyo basi, tafakari ni uzoefu wa nguvu ya Upendo wa Mungu unaombadilisha kabisa mtu na kumfanya aliye mdhaifu katika kufikiri mambo matakatifu na kupenda, aweze kufanya hivyo kwa njia ya kimungu zaidi. Kwa uhalisia wa ubinadamu wetu, kila mmoja anahitaji kuguswa na Mungu.



Tafakari au taamuli ina thamani kubwa sana katika maisha ya kila Mkristo. Ndiyo maana kwa Wakarmeli, tafakari si kwamba ni chemchemi ya maisha ya kiroho tu, bali pia ndiyo inayoamua na kusaidia ubora wa maisha ya kindugu na ya utumishi kwa watu wa Mungu. Kwa lugha nyingine, karama ya tafakari ndiyo inayoziunganisha karama nyingine mbili.

Wakarmeli popote walipo, wanapofanikiwa kuyaishi kwa uaminifu matunda yatokanayo na tafakari, pamoja na kuwa katikati ya maisha yenye changamoto za kila aina, basi huo huwa ndiyo ushuhuda wa fumbo la uwepo hai wa Mungu  kati ya watu wake. Mkristo hatakiwi kujenga kisingizio chochote cha kutopata muda wa kukaa na kuongea na Mungu.



Ndiyo maana kazi ya kuutafuta uso wa Mungu na upokeaji wa zawadi za Roho Mtakatifu inazifanya jumuiya za Wakarmeli kuwa angalifu zaidi katika kuzitambua alama za nyakati na wakati huo huo  kuwa makini zaidi katika kuzitambua mbegu za Neno wa Mungu.



Hapo ndipo unapokuja kugundua kuwa maisha ya taamuli au tafakari huzingatia na hutathmini matukio mbalimbali ya kihistoria yatokeayo ndani ya Kanisa, duniani na sana sana katika jamii za watu wa kawaida, kwa lengo la kutoa msaada unaohitaji kulingana na mapenzi ya Mungu.



Kwa njia hiyo basi Wakarmeli kwa kumfuata Yesu Kristo, huonyesha mshikamano kwa kuhamasisha matukio yaletayo matumaini na upendo katika jamii. Kwa kuyatafakari yote yanayotokea katika ulimwengu huu, na kwa kuongozwa na Neno la Mungu, Wakarmeli hujitahidi kufanya maamuzi ambayo huchangia kuyabadili maisha ya watu wengi ili maisha na matendo yao yalingane na mapenzi ya Mungu Baba.



Nirudie kusisitiza kuwa, ili maisha ya taamuli –tafakari yaweze kuzaa matunda, hutakiwa ukimya wa kweli wa ndani ambao humpa nafasi Mungu ya kuongea. Kutokana na kuhitajika kwa ukimya wa ndani hata mazingira ya nje hutakiwa yawe ya ukimya pia. Ukimya wa nje hurahisisha zoezi la kuzama ndani kabisa mwa nafsi na kuungana na Mungu. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.

Home

Kundi la Wakarmeli Watanzania wa kwanza lililofungua misheni 2009 Bikira Maria na Nabii Eliya katika Karmeli