MWITO WA MUNGU KATIKA HISTORIA YA MWANADAMU
1. Utangulizi
Mwanadamu hakuumbwa ili ajipe kila kitu au ajikamilishe yeye mwenyewe.
Kuwa mwanadamu inamaanisha kuilekea hali iliyo juu yetu na kubwa kuliko ya
kwetu. Hiyo hali ndiyo tunayoitafuta, au kwa lugha nzuri zaidi, huyo ndiye
tunayemtafuta ili tukutane naye na kumpenda. Ili hali hiyo tuweze kuziishi
ndipo hapo tunapokuja kujua tunu mbili za maisha ya utawa: (i) kumwiga Kristo na (ii) kukutana na Mungu. Ili hilo liweze kuzaa matunda ni lazima kuwepo na wito.
Sasa wito ni nini?
2. Wito
Neno wito linafanana na neno la kilatini «vocatio» likiwa na maana ya “mwito au mwaliko”. Hii
nayo inatokana na kitenzi, «vocare», ikiwa na maana ya «ita». Ni mwelekeo wa ndani ya nafsi wa kupenda
kitu fulani au maisha fulani. Roho inapoelekea. Hii inatafsiriwa kama sauti (vox) inayosikika ndani ya nafsi ya mtu. Ndipo
hapo tunakutana na neno mwito au wito. Katika nyanja ya maisha ya kitawa
tunasema: “mwanadamu ameitwa na Mungu kuishi
maisha ya kitawa”. Kama sauti hii, mwelekeo huu umo ndani yetu, basi ina
maana kuna aliyeuweka. Naye ni Mungu. Mungu ndiye anayeita. Mungu humwita mtu
kwa jina (Is 45:3), mwito wake hauwezi kuujutia (Rum 11:29), kila mtu kaitwa
peke yake (Yoh 21:22). Mwito wa Mungu ni kuitwa katika maisha kuingia maishani, ni mwito wa wokovu, ni mwito wa utakatifu, ni mwito wa kuingia katika muungano au usharika na Mungu.
Hivyo wito ni kazi ya Mungu. Nao una sifa zifuatazo:
a) Mwito ni fumbo. Chanzo chake ni Mungu.
b) Kila mtu kaitwa kwa namna yake, (kivyake).
c) Ni majadiliano ya upendo kati ya mtu na mwanadamu.
d) Ni zawadi ya upendo.
e) Ni Mungu anayejiweka karibu na mwanadamu.
f) Ni kuongoka.
g)
Ni kufanya experience mpya ya maisha.
h)
Ni kuuelekea ukamilifu wa maisha.
3. Nifanyeje kuitikia mwito wa Mungu?
1.
Kitu cha kwanza ni kuona kuwa na uwezo wa
kuyatafakari mambo yote yanayotokea na yanayogusa maisha yako mwenyewe. Jaribu
kuingia katika ulimwengu wako wa ndani na kuona jinsi ulivyo na unavyoishi leo katika uhusiano wako na Mungu.
2. Kitu
cha pili uwe na uwezo wa kueleza hali yako ya ndani. Ndani mwako kuna nguvu
zinazokuvuta kuelekea maisha yapi? Chukua diary
yako ya kiroho jaribu kuandika matukio ya ndani. Unavutwa na maisha ya
watakatifu? Unavutwa na maneno na maisha ya Yesu? Au unavutwa na nini?
3. Jibidishe kusali sala binafsi. Sala zitakusaidia kufikia uamuzi muhimu na makini
katika maisha yako na hivyo kutoa jibu sahihi. Sala inayokupeleka katika
usikivu wa ndani.
4. Jibidishe
kujifahamu. Yasome maisha yako kwa makini. Unahisi kama Mungu ana mpango wowote na wewe? Una hofu?, ndani mwako una
machafuko? Unatambua udhaifu wako? Je hayo
yote kwako yana maana gani? Ni kikwazo au ni faida?
5. Jifungue
kwa Mungu, kubali yanayotokea (Flp 2:5-7). Acha kile
kitu unachokita hasa katika maisha kiwe wazi na tumaini ulimwengu
uliobora
zaidi. Kila siku acha sauti ya Mungu iongee ndani mwako. Sauti hiyo
ilishe neno la Mungu kila siku. Soma Biblia ili uweze kujua mapenzi ya
Mungu. Kuwa mfano
wa mtumishi. Achana na fahali za kidunia ambata na mtumishi mnyenyekevu
Yesu Kristo.
6. Hatua ya mwisho ni kuamua. Kinachoweza kukwamisha uamuzi ni hofu ya
kukosea wito. Uamuzi unaangalia unachojifahamu leo. Unapima mahitaji ya
wito na kuyajua yalivyo na kujipima leo. Maamuzi ya wito ni kuamini kuwa Mungu
atakuongoza kwa maisha yako yote. Ni kuamini kuwa siku kwa siku anafanya kazi
na kuishi pamoja na wewe na kuamini kuwa anaweza. Mfani ni wa Abramu, aliitwa
akaenda pasipokujua alipokuwa anakwenda (Ebr 11:8). Jambo hili linatokana na
swali la msingi, Mungu ni nani kwangu?
7. Hitimisho. Ni kuacha yote na kumfuata Yesu
Kristo. Swali litakuja. Naweza? Jibu tunalipata kutoka kwa Yesu anaposema. «Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi
niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu
yapate kukaa» (Yoh 15:16).
8. Inabidi uelewe kuwa katika wito huu,
utamtumikia Mungu vizuri, utajitakatifuza na kutakatifuzwa na kupata wokovu, na
utafanya kazi kwa ajili ya wokovu wa watu wengine nay a kuwa utamtukuza Mungu.
4.0. Kukua katika wito
Kuishi kadiri ya tunu (values)
za wito. Hapa kuna swali la msingi
ambalo kila mmoja anatakiwa ajiulize. Nalo ni hili: Utafanyaje ili ukue katika wito
wako na utatambuaje kuwa unakua? Hapa kinachoangaliwa ni uwepo wa tunu za wito na sababu zake.
4.1. Tabia. Kitu cha kwanza
kinachoangaliwa na watu wengi ni tabia.
Mfano, anasali, nimwema, ni mpole, ni mtii, anakaa
vizuri na watu, anajua kufundisha vizuri dini. Kwa vipimo hivyo mara nyingi
husema huyu atakuwa au Padre (Mtawa) mzuri au sisita mzuri. Na wanahitimisha
kwa kusema kuwa ana wito. Hivyo kwa
vigezo hivyo tabia inakuwa ni
kielelezo cha tunu za wito. Kinachotakiwa ni kuzifanya tunu
hizi ziwe na sababu ya ndani iliyo njema. Hivyo inabidi kujiuliza maswali haya:
kwa nini unasali?, kwa nini unatii?, kwa
nini unapenda kukaa na watu?............n.k. unafanya hivyo kwa sababu ya tunu
za wito au kwa sababu ya mahitaji yako mwenyewe ya kibinadamu?
Mfano kuna watu wanaonekana ni
watii kwa kila kitu kumbe ni hofu ya kuogopa kuchukua majukumu mengine ya
maisha. Unaweza kukaa na watu kwa ajili ya upendo na huduma lakini vile vile
unaweza kukaa nao kwa kutafuta kusifiwa
na kushukuriwa. Tabia ya nje ni nzuri
lakini sababu ya ndani ni kinyume.
Hivyo kinachoangaliwa ni kwa kiasi gani tunu hizo unazoziishi zitakuwa sehemu
kweli ya maisha yako ya ndani ya wito wake.
4.2 Tunu na kazi
Ili kutambua kuwa mtu anakua
katika wito huangalia jinsi anavyopokea kazi
na majukumu mengine. Hapa tunaangalia
majukumu na nafasi wanayopewa watawa katika jamii. Majukumu haya humsaidia mtu
kuzimwilisha tunu za wito na hivyo kukua, kutoka kwenye eneo la mahitaji binafsi na kuyafanya mahitaji ya kiwito. Inabidi kuwa makini
sana na kazi tuzifanyazo. Mtu anaweza kufanya kazi nyingi sana na za kufaa,
lakini akija katika sala, hasali. Hili ni jambo la hatari sana katika maisha ya
kitawa. Hivyo neno kukua lina maana ya
kuzibadilisha tunu zote na kuzifanya kuwa za kiwito. Hizo huonekana katika
ishara tatu:
i. Kazi ni kielelezo cha tunu kama
limechaguliwa si kwa kujifurahisha bali kwa ajili ya umuhimu wake. Kuwa na imani kuwa kitu hiki ni muhimu.
ii. Kazi ni kielelezo cha tunu ikiwa aliyechagua
kazi anafungamana nayo na kudumu katika huduma ya kitume bila kulalamika. Mfano
kufundisha ni tunu, lakini pale mtu anapoifanya kazi ya kufundisha kama ndio msingi wa kuwa katika utawa, hapo kuna
kuchanganya mambo. Mtu wa namna hiyo yuko tayari kuziweka pembeni nadhiri za
kitawa. Kwake kikubwa si nadhiri bali kufundisha tu basi! Ikiwa ataambiwa aache
kufundisha anajisikia kupoteza wito!
Mtu anayefanya kazi kwa tunu
anakuwa huru ndani kufanya kazi yoyote.
iii. Na ya tatu ni pale ambapo kazi inafanywa
kama njia ya maisha na si kama lengo la maisha. Kuna kazi ambazo humtaka mtu
ajikatalie. Yesu anasema kujikana. Kama mtawa anaishi tunu hii, yuko tayari kwa
lolote kulinda wito wake na tunu zake. Kinyume chake yuko hatarini kukata
tamaa. Mwisho anaweza kuamua kuendelea na mtindo wake wa maisha na kufanya
anavyoona yeye. Matokeo yake ni kufanya bila upendo. (1Kor 13:1-13).
4.3 Mungu ana nia maalum nawe.
Mungu anapomwita mtu, mtu huyo
hubadilika kabisa. Hawezi kuishi kama alivyokuwa mwanzo. Kuitwa kwa mtu, ni
kitu binafsi mno. Mungu alipomwita Ibrahimu hakuwaza au kufikiri, kilikuwa ni
kitendo cha kipekee: «Bwana
akamwambia Abramu, “Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya
baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonesha”...(Mwa 12:1)». Abramu
aliisikia sauti ya Mungu katika dhamira yake akafanya kama Mungu alivyomwagiza.
Musa alikuwa anachunga kundi la
mkwewe Mungu alipomwita kutoka kwenye kijiti cha moto (Kut 3:4). Mungu alimwita
kijana Samweli, akimtaka kuwa tayari kupokea jukumu la kuibadili siasa ya
utawala wa Israeli, (1Sam 3:1-21). Eliya
alisikia sauti ya Mungu kwenye upepo mororo (1Fal 19:12-13). Kuna kipindi sauti
ya Mungu inasikika hata kwenye keleke nyingi ikiwa anayeitwa atasikiliza kwa
makini. Sauli (Paulo) (Mdo 9:1-4).
3. Mt. Agostino
Alivyokuwa na akili na nia ya
kumtafuta Mungu. Kwa sala za mama yake Monica alifanikiwa kumjua na kumpokea
Kristo akabadilika kabisa katika maisha yake.
4. Wito ni upendo wa Mungu unaojifungua ndani ya mwanadamu
Wito ni onesho la upendo Mungu
unaopita vitu vyote na ambao huufanya moyo wa mwanadamu uwe wazi kwa ajili ya
mambo ya Mungu. Mtu hubadilika na kuwa zawadi ya upendo kwa wengine na kwa
maisha yake yote. Mwanadamu anayeitwa anaweza kukubali lakini vile vile yuko
huru kuukataa huo upendo. Daima mwanadamu anapendwa na kuitwa na Mungu.
Anachotakiwa kufanya ni kujiachilia mikononi mwake. Historia ya wito wa mwanadamu inaanzia kwenye
uumbaji (Mwa 1-2) na itakamilika nyakati za mwisho ambapo kila kitu
kitajumuishwa ndani ya Kristo (Efe 1:10).
5. Uaminifu wa mwanadamu anayeitwa na Mungu
Mungu huonekana mwaminifu kwa Mungu anapoushinda ubinadamu wake.
anayeonekana na mwaminifu ni yule anayetegemea kuyaweza yote kwa msaada wa
Mungu. Ukweli huu, hujionesha jinsi anavyotenga muda wake kwa ajili ya kuongea
na Mungu.
6. Miito katika Agano la Kale-Wito wa Israeli na manabii
Tunapoongelea miito katika
Agano la Kale, hasa tunalenga uhusiano wa kuteuliwa kwa upendo kwa taifa la
Israeli. Kwa hiyo katika kuitwa kuna
dhana nzima ya kuteuliwa, au kuchaguliwa.
Mungu alifanya nao agano katika mlima Sinai ili wawe wajumbe wake kwa wengine.
Ili kulidhibitisha hilo anawaita wazaliwa wa kwanza pale alipomtuma Musa
awaokoe kutoka utumwani Misri, (Kut 4:22). Kati ya mataifa wao watakuwa ufalme
wa makuhani, (Kut 19:6).
6.1. Majibu ya mwanadamu kwa Mungu
Mungu anapomwita mwanadamu
huwa anasubiri majibu. Maneno yanayotumika kuonesha majibu yanayotakikana na
haya: «isikilize sauti», «litunze agano la Mungu».
Mfano taifa la Israeli linamjibu Mungu kwa kusema «Watu
wote wakaitika pamoja wakasema, “Hayo yote aliyoyasema Bwana tutatenda”»,
(Kut 19:8a). Kilichowajenga kama taifa takatifu ni uhusiano mwema na Muumba wao,
yaani, walitakiwa wajitenge na kila kitu ambacho hakiambatani na maisha ya
kimungu. Hivyo wito halisi wa
mwanadamu ni utakatifu. Mungu
anamwita kila mwanadamu kuwa mtakatifu. Katika kuitikia wito wa utakatifu, huwa
tunaitikia wito wa wokovu kwa kuishi ama maisha ya kitawa, ndoa, kipadri ama
kuishi mwenyewe, lakini yote iwe ni kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Ndipo hapo
unakuta kila mtu anaitikia wito mkuu wa
utakatifu kwa jinsi alivyoitwa kwa maisha mbalimbali. Mtume Paulo anasema:
«Kila mtu na akae katika hali ileile ambayo alikuwa nayo alipoitwa» (1Kor
7:20).
6.2. Wito wa manabii
Mungu alikuwa akiongea nao ndani ya dhamira zao. Tunapoangalia historia yao
ya kuitwa tunaona karibia kila nabii aliweka kwanza ukinzani kabla ya kukubali. Hasa kilichowafanya kutokubali kirahisi
ni kutambua udhaifu wao wa kibinadamu (Is 6:5), na kuhisi ugumu wa kufanikiwa
katika misheni zao. walitambua kuwa kazi ya kinabii, mwisho wa siku haitawapa
heshima yoyote mbele ya jamii, au faida binafsi, tena kinyume chake wataonekana
kichekesho mbele ya jamii au adui! (Is 8:11-15), (Yer 15:10).
4. Kutwa kwa Mitume
Yesu alipoanza kazi yake ya kuhubiri, alianza kuwaita watu mmoja mmoja
ili wawe naye na wamfuate. Hawa ndio wale waliofahamika kama wanafunzi wake.
Miongoni mwao alichagua kundi la watu kumi na wawili ambao ndio Mitume. Hawa
ndio wale walioambatana naye katika kazi yake. Tukio la kuwachagua lilikuwa ni
tukio kubwa kiasi kwamba kabla ya kulifanya alisali. Mwinjili Luka anasema
hivi: “Ikawa siku zile aliondoka akaenda
mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata kulipokuwa
mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao ambao
aliwaita Mitume”. (Lk 6:12-13; Mk 3:13-19).
5. Kwa nini Yesu aliwaita hawa Mitume?
Jibu
tunalipata kutoka kwa Mwinjili Marko anaposema: “Akapanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akawaweka
watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena
wawe na amri ya kutoa pepo”. (Mk 3:13-15).
Aya mbalimbali za kuitwa katika Biblia.
Rum 8:29-30. Rum 9:11.
1Kor 1:4-9.
1The 2:12. 1The 5:24.
Gal 1:6.
Efe 1:18.
1Pt 1:15; 1Pt 2:9.
1Pt 5:10.
3. Kitu muhimu katika kuitwa kwao
Kwanza iliwabidi wakae naye, wamfahamu yeye binafsi na kufahamu
kilichomleta ndipo hapo watumwe. Aliwaandaa ili wakalihubiri Neno. Hivyo
walitakiwa watumwe, ndio maana wanaitwa Mitume.
Yaani, waliotumwa. Ilibidi awaandae yeye mwenyewe na kuwapa mamlaka dhidi ya
nguvu za mwovu. Haya ni mamlaka ya kimungu. (Mk 3:15).
5. Umuhimu wa Mitume
Mitume walikuwa
na kazi muhimu sana katika maisha ya Yesu. Mmoja wao, Yuda, alimsaliti lakini wengine walibaki waaminifu
kwa Yesu. Hawa ndio wale waliotoa ushuhuda juu ya yote aliyoyaisha na
kuyafanya. Baada ya kifo na ufufuko wake Mitume walitiwa nguvu na Roho
Mtakatifu wakaanza kuhubiri. Walieleza Yesu alikuwa nani na alifanya nini. Bila
wao ujumbe wa Yesu usingesambaa duniani. Kuitwa kwao lilikuwa jambo kubwa na
muhimu sana kwa ajili ya wokovu wa watu wengine.
6. Umuhimu wa kuitwa leo
Hata nyakati zetu, kuitwa ni kitu muhimu sana katika maisha. Mungu
anaendelea kuwatumia watu wanaume kwa wanawake kuendeleza kazi ya Yesu
iliyomleta duniani. Jambo hilo linategemea utayari
wa nafsi ya mtu. Sauti ya Mungu inaita kutoka ndani mwa mtu ikimtaka aishi
maisha fulani, kwetu sisi ni maisha ya utawa. Kuwa tayari kuacha yote kama
Mitume na kuambatana na Yesu popote anakapotupeleka (Mk 10:28).

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.